Skip to main content

Diwani Akwepa Risasi sita akipambana na majambazi Moshi


MTU KWAO BLOG /01
Diwani wa Kata ya Kiborlon (Chadema) katika Manispaa ya Moshi, Frank Kagoma ameonyesha ujasiri wa hali ya juu alipopambana na majambazi waliokuwa na silaha za moto.
 Alinusurika kuuawa baada ya majambazi hao waliokuwa na bunduki na bastola kumfyatulia risasi sita alipokuwa akiwafukuza ambazo hata hivyo, hazikumpata.
Tukio hilo ambalo lilionekana kama sinema, lilitokea mwishoni mwa wiki baada ya majambazi hao kuvamia duka la jumla la kuuza mitumba linalomilikiwa na Menti Mbowe na kupora Sh10 milioni.
Katika tukio hilo lililotokea saa tano asubuhi eneo la Kiborlon, majambazi hao walimjeruhi kichwani mfanyabiashara huyo anayemiliki pia mabasi ya Machame Safaris.
Hali ya majeruhi huyo inaendelea vizuri. Akisimulia tukio hilo, diwani huyo alisema siku hiyo akiwa maeneo ya Kiborlon, alipigiwa simu kuwa mfanyabiashara huyo amevamiwa na majambazi ndipo alipoendesha gari lake hadi eneo la tukio.
“Nilipofika pale wale majambazi watatu ndiyo walikuwa wanatoka kwenye duka. Nikampelekea gari yule aliyekuwa ameshika bunduki. Kuona hivyo akafyatua risasi hewani,” alisema Kagoma.
“Yule mwenye bunduki akaingia uchochoroni kuelekea Barabara ya Stendi ya Kidia. Mwenzake aliyekuwa na bastola naye akawasha risasi nyingine hewani kunitisha,” alisema.
Baada ya hali hiyo, diwani huyo alilazimika  kujificha kwenye gari na majambazi hao walidandia pikipiki na kuanza kukimbia kuelekea Barabara ya Msaranga, naye akawafuata kuelekea huko.
“Wakati huo tayari vijana wangu wa bodaboda wakawa nao wamesikia hilo tukio tukaanza kusaidiana kuwafukuza lakini mbele kidogo pale Msaranga wale majambazi wakasimamisha pikipiki yao umbali wa mita 30 kutoka nilipokuwa na mmoja wao mwenye bunduki alifyatua risasi mbili na mwenye bastola risasi mbili kuelekea uelekeo wangu.
“Nililazimika kujificha kwenye kiti, wale majambazi wakajua wameniua. Wakapanda tena pikipiki ili watoroke. Nikawasha tena gari huku vijana wangu nao wakinisaidia tukaanza kuwafukuza,” alisema.
Kagoma alisema majambazi hao walipita maeneo ambayo gari haliwezi kupita wakaelekea eneo la Mabogini Moshi Vijijini hadi lango la TPC na baadaye wakaelekea Rundugai wilayani Hai.
“Kuna eneo vijana wangu wanasema kulikuwa na vumbi sana, ndipo walipowapoteza na majambazi wakatoroka kupitia njia ya reli ili kukwepa polisi waliokuwa wakiwasubiri mbele,” alisema na kuongeza: “Hatukuwa na silaha, lakini tulijitahidi kupambana nao kwa ujasiri. Tatizo nafikiri tulikosea kidogo. Ilitakiwa wakati tukifukuzana nao tuwape polisi uelekeo wa majambazi.”
Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa alisema jana kuwa Jeshi lake litatoa taarifa rasmi kwa wanahabari leo kuhusiana na msako unaoendeshwa na jeshi hilo.
“Kuna mambo tumeyafanya tangu tukio hilo litokee lakini kesho (leo) saa sita mchana tutatoa taarifa rasmi pamoja na mafanikio tuliyofikia hadi sasa. Tunaendelea vizuri na upelelezi,” alisema.
Kamanda Mutafungwa, alitoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo ikiwamo kuwafichua wahalifu na mbinu wanazozitua akisema polisi wamejipanga kukabili wimbi jipya la ujambazi.

Comments

Popular posts from this blog

Kifafa cha Mimba (Preeclampsia, eclampsia)

MTU KWAO BLOG / Eagle Eyes Kifafa cha mimba ni ugonjwa unaohusiana na msukumo mkubwa wa damu (high blood pressure) wakati wa ujauzito pamoja na kuharibika kwa viungo muhimu mwilini kama vile figo na ini. Kwa kawaida ugonjwa huu hutokea baada ya nusu ya kwanza ya ujauzito kuisha (kuanzia wiki ya 20 au miezi mitano ya ujauzito). Ugonjwa huu huweza kuwatokea hata wajawazito ambao hawakuwa na tatizo la msukumo mkubwa wa damu kabla ya ujauzito. Ugonjwa wa kifafa cha mimba unaweza kuleta madhara makubwa kwa mjamzito na mtoto aliye tumboni. Kuharibika kwa viungo muhimu kama figo na ini la mjamzito kunaweza kuwa kwa kiwango kikubwa kichoweza kusababisha mjamzito kupoteza maisha iwapo hatapata huduma ya afya mapema. Vilevile mtoto aliye tumboni anaweza kuathirika kwa kukosa damu ya kutosha toka kwa mama na kushindwa kukua vizuri na iwapo hali hiyo ikiendelea muda mrefu anaweza kufia tumboni. Kutokana na hatari kubwa ya ugonjwa huu kwa wajawazito na watoto walio tumboni, ina...

Medical gamble that saved a little boy’s life

  The 18-month old boy was rushed to Muhimbili National Hospital (MNH) in Dar es Salaam where he was admitted. But his condition soon deteriorated into acute kidney failure. A dark cloud hovered over the family. The country’s biggest referral hospital has for years been infamous for being too ill-equipped to save those dying from such conditions. To read the whole story click here

Haya ndiyo madhara ya Kutumia earphones

Imeelezwa kuwa watu wanaotumia redio za simu wako hatarini kupatwa na ugonjwa wa saratani ya sikio na kichwa kutokana na mionzi mikali itokanayo na viselula hivyo. Akizungumza na FICHUO TZ, Dk. Leopard Mwinuka alisema, watakaoathirika na tatizo hilo ni wanaotumia muda mwingi kusikiliza redio ama muziki kwa kutumia spika za masikioni ‘headphone’. “Nawaonea huruma wanaotumia muda mwingi kusikiliza redio ama muziki kwa kutumia spika za masikio, kwani madhara yake hawawezi kuyaona sasa bali siku zijazo watapata ugonjwa wa saratani,” alisema Dk. Mwinuka. Alimaliza kwa kusema kuwa, mbali na kupata ugonjwa huo, wahusika wanaweza kupata tatizo la kutosikia vizuri kwa sababu, mtu anapotumia spika za sikio huweka sauti kubwa ili apate mdundo mzuri baada ya muda ngoma ya sikio inaathiriwa na hali hiyo. Habari nyingine za kitabibu zilisema kwamba, kwa kuwa pande zote za spika zina sumaku, huweza kuvutana na kuvuruga mpangilio wa ubongo hasa kama spika hizo zitakaa maskioni kwa zaidi ya sa...